Monday, 28 November 2016
MAHAFALI YA PILI SHULE YA SEKONDARI MGUTWA SIMANJIRO
Meneja wa shule ya sekondari Mgutwa ya Kijiji cha Kandasikira, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Monica Mlemeta akizungumza kwenye mahafali, (wa pili kushoto) ni mgeni rasmi Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga, Kazimbaya Makwega na Mkurugenzi wa taasisi ya Agape Mission International inayomiliki shule hiyo Canon Kedmon Mlemeta.
Wanafunzi 65 wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Mgutwa inayomilikiwa na taasisi ya Agape Mission International, iliyopo Kijiji cha Kandasikira Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye mahafali ya pili ya shule hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga, Kazimbaya Makwega, akimpa zawadi mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mgutwa iliyopo Kijiji cha Kandasikira, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Isack Chacha, kwenye mahafali ya shule hiyo, kushoto ni meneja wa shule hiyo Monica Mlemeta na wapili kulia ni Mkurugenzi wa taasisi ya Agape Mission inayomiliki shule hiyo Canon Kedmon Mlemeta.
SHAKA AFANYA ZIARA SIMANJIRO
Kaimu Katibu Mkuu
wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka akiwa na Kamanda wa UVCCM wa Wilaya ya Simanjiro
Mkoani Manyara, Daniel Ole Materi kwenye Kijiji cha Loiborsoit A, Kata ya
Emboreet, alipofanya ziara yake ya siku mbili wilayani humo.
Thursday, 13 October 2016
WANYONGE KULIPIWA MATIBABU YA iCHF HANANG'
Wananchi wanyonge ambao ni kaya masikini wamenufaika baada ya Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, George Bajuta, kujitolea
sh1.8 milioni kwa ajili ya kuzilipia kaya masikini 36 za watu 216 wa Kata ya
Simbay kwenye mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa (iCHF).
Bajuta ambaye ni
diwani wa kata hiyo aliyasema hayo kwenye uzinduzi wa mfuko wa afya ya jamii
ulioboreshwa (iCHF) ulioandaliwa na mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF)
mkoani humo na kudai kuwa kila kitongoji kitatoa kaya tatu za wanyonge wasiojiweza.
Alisema kata yake
ina vitongoji 12 na kila kitongoji kitachagua kaya tatu ambazo ni familia
za wanyonge zisizojiweza ili awalipie sh30,000 kila kaya yenye watu sita, baba, mama na
watoto wanne, zitakazopata huduma za afya kwa mwaka mzima.
“Mimi sina
utajiri mkubwa ila nimeamua kujitolea kidogo nilichonacho kwa kuhakikisha wale
ndugu zangu wanyonge wasiokuwa na uwezo kabisa kwenye kila kitongoji nao wapate fursa ya
kutibiwa bure kwa mwaka,” alisema Bajuta.
Mkuu wa wilaya
hiyo Sarah Msafiri akizungumza wakati akizindua mfuko huo alisema wananchi wa
eneo hilo wanapaswa kushiriki ipasavyo kwa kujiunga na (iCHF) kwani hadi mwisho
wa mwaka inatakiwa asilimia 50 ya watu wajiunge.
“Hapa kwenye Tarafa
ya Simbay kuna zaidi ya wakazi 6,200 hivyo tunapaswa kujiunga kwa wingi ili watu
zaidi ya 3,100 ambayo ndiyo nusu ya watu ili kutimiza lengo la serikali la
kuhakikisha hadi idadi hiyo inafika,” alisema Msafiri.
Meneja wa mfuko
wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani Manyara, Isaya Shekifu alisema kila kaya
itakayotoa sh30,000 kwa ajili ya kuchangia mfuko huo nayo serikali kuu
huchangia nusu nyingine sh30,000 na kuwa sh60,000.
Shekifu alisema iCHF
iliyoboreshwa inajenga mfuko endelevu wa kuchangia kijamii gharama za matibabu
na kuboresha ubora wa huduma za afya kupitia mafunzo kwa watoa huduma, utoaji
vifaa tiba na uboreshaji miundombinu ya huduma.
CRDB YAKABIDHI HOSPITALI YA HAYDOM MASHUKA 100
Benki ya CRDB imetoa msaada wa mashuka 100 kwenye hospitali
ya rufaa ya Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, kwa lengo la kuwasaidia
wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo inayohudumia zaidi ya watu wa mikoa minne
nchini.
Akizungumza wakati akikabidhi mashuka hayo 100 kwa
mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Emanuel Nuwass, Meneja wa CRDB Tawi la Babati
Ronald Paul alisema wanatoa msaada huo ili kurudisha hisani kwa jamii.
Paul alisema wamekabidhi mashuka hayo ili kutoa asante kwa jamii
kwenye wiki ya huduma kwa wateja, kwa kurudisha kwao kile kidogo wanachopata
kwa ajili ya kuboresha mahusiano zaidi baina ya benki hiyo na wateja wake.
“Tutaendelea kushirikiana na kusaidiana kwenye masuala
mbalimbali ya kijamii kwani tunatambua jitihada na changamoto ya hospitali ya
Haydom ambayo inatoa huduma kwa watu wa Manyara na waliopo mikoa ya jirani,”
alisema.
Hata hivyo, mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Emanuel Nuwass
alisema hii ni mara ya tatu kwa benki hiyo kutoa msaada kwenye hospitali ya
Haydom, hivyo iendelee kuwa karibu nao kwa ajili ya kupeana ushirikiano wa
kusaidia jamii.
Dk Nuwass alisema awali benki hiyo ilitoa mchango wa
maendeleo wa sh1 milioni kwa ajili ya siku ya Haydom, kisha wakawapa zawadi ya
ng’ombe mmoja mkubwa wa siku ya familia na mashuka 100 yatakayotumiwa na
wagonjwa.
Alisema hivi karibuni bodi ya hospitali hiyo ilikubaliana na
mpango wa malipo kwa wagonjwa kupitia njia ya kadi ya CRDB na zoezi hilo
linatarajia kuwarahisishia watu wote watakaopata huduma katika eneo hilo la
Haydom.
Kwa upande wake, meneja masoko mwandamizi wa benki hiyo
Fredrick Siwale alisema benki hiyo itandelea kutoa huduma nzuri kwa wateja wao
huku ikiboresha maeneo ambayo huduma haipatikani kwa kuhakikisha wanakuwepo.
“Kupitia kauli mbiu yetu ya ulipo tupo kama hatupo tutakuja
na kama hatujaja utusubiri, tunalenga kuwahudumia watanzania wote na kupitia
hilo ndiyo sababu tukafika kutoa mashuka haya kwani tunaithamini jamii,”
alisema Siwale.
CRDB YATOA MIKOPO YA SH16.1 BILIONI MKOANI MANYARA
Benki
ya CRDB Tawi la Babati Mkoani Manyara, imefanikiwa kutoa mikopo ya
sh16.1 bilioni kwa wajasiriamali, watumishi wa Serikali, watumishi wa
sekta binafsi, vyama vya kuweka na kukopa na asasi za fedha.
Watumishi
wa serikali na wasekta binafsi 1,604 walikopeshwa sh12.8 bilioni na
wajasiriamali 84 walikopa sh3.3 bilioni ikiwa ni pamoja na
wafanyabiashara na wakulima.
Meneja
wa benki ya CRDB Tawi la Babati, Ronald Paul akizungumza kwenye
kilele cha wiki ya huduma kwa wateja, alisema wamedhamiria kuwapa wateja
wao huduma bora na kuwanyanyua kiuchumi.
Paul
alisema kwa muda wa miaka miwili tangu waanzishe huduma ya benki hiyo
mkoani Manyara, wamefanikiwa kufungua matawi mengine madogo wilaya za
Mbulu, Hanang, Simanjiro na Kiteto.
Alisema
pia wamefanikiwa kufungua huduma za matawi madogo yaliyopo Magugu,
Haydom na Mirerani ambayo kupitia hayo wameweza kupata akaunti za
halmashauri za wilaya.
Alisema
kwenye matawi yao madogo wamefanikiwa kuwa na huduma za ATM ambazo
wamefungua 10 kwenye mkoa huo na zinafanya kazi kwa muda wa saa 24.
"Kwa
kipindi hiki tumefanikiwa kuongeza ajira kwa watanzania hususani kwa
wana Manyara kutoka wafanyakazi 12 hadi 37 kutokana na matawi mengine
madogo yaliyofunguliwa katika wilaya mbalimbali," alisema.
Alisema
wamefanikiwa kupata amana za sh11 bilioni zilizotokana na wateja 12,000
waliofungua akaunti za akiba, watoto jumbo, akaunti za malkia, akaunti
maalum, bidhaa nyingi za kibenki za Simbanking, ATM na fahari huduma.
Mkurugenzi
wa mji wa Babati Fortunatus Fwema alitoa wito kwa benki hiyo
kuwatafutia wateja wa mbaazi wa nje ya nchi kwani hivi sasa wakulima
wengi wanapata changamoto ya soko la zao hilo.
Fwema
alisema kutokana na benki hiyo kutoa huduma za fedha hadi nje ya nchi
hasa nchini India, wangetumia fursa hiyo kwa kuwaunganisha wakulima hao
moja kwa moja na soko la mbaazi ambalo wanunuzi wengi hutoka nchini
India.
Subscribe to:
Posts (Atom)